Main Sponsor

MAKALA: MAAMUZI MAGUMU YAMEWALIPA SINGIDA BIG STARS

Na Kiepo Benedicto

 

Labda mpaka sasa kila mtu anaijua nia na lengo la Singida Big Stars, hii ni mara baada ya kushuhudia ubora wa timu waliyokuwa nayo ukichagizwa na usajili na maamuzi magumu waliyoyachukua kwa manufaa ya timu hiyo.

Safari ya kujiuliza hii ni timu ya aina gani ilianza toka msimu ambao ilijiandaa kupanda ligi kuu Bara. Wakati huo ikiitwa DTB (Diamond Trust Bank). Klabu hiyo ilifanya usajili mastaa wenye majina makubwa na waliowahi kuhudumu hapa nchini kwenye vilabu vikubwa.

 

Maamuzi magumu yalianzia hapa, hapa yalifanywa maamuzi magumu kifedha. Wakati vilabu vingine vikihofia na hata kushindwa kuwaleta mastaa tishio kwenye vilabu vyao, wao wakafanya hivyo.

 

Walimrudisha nchini James Kotei, wakamleta Nicholas Gyan, wakaongeza nguvu ya Amissi Tambwe na wengineo lengo likiwa ni kupanda Ligi Kuu. Unadhani walitumia pesa kiasi gani kuhakikisha wanawaleta mastaa ambao watawasaidia kupanda Ligu Kuu? Vipi kama wasingefanikiwa? Ndio maana nakuandikia hapa yalikuwa maamuzi magumu kuyafanya lakini yamewalipa sana.

 

Walivyopanda ligi kuu Tanzania Bara wakaona isiwe tabu, njia tuliyotumia kupanda Ligi Kuu Bara ndio itakayotumika pia kujiweka mahali pazuri katika ligi hii. Sasa ile tafsiri ya maamuzi magumu inajidhihirsha tena hapa.

 

Kiufundi, Singida ilifanya maamuzi magumu mara baada ya kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara wakafanya usajili wa mastaa mbalimbali ambao wengine walitemwa na vilabu vingine vya ligi kuu Bara. Wakati usajili unafanyika kila mtu alikuwa anawaza hivi hawa wachezaji walionesha kupungua viwango walikokuwepo watafanya nini Singida? Ndivyo inakupasa uelewe maamuzi yalikuwa magumu kuwachukua Medie Kagere, Deus Kaseke, Paschal Wawa na wengineo walioonesha kufeli kiasi cha vilabu vyao kuachana navyo. Lakini hao hii leo wamewafanya wasalie kama miongoni mwa timu bora ndani ya ligi yetu ikishika nafasi ya nne kwenye ligi na kuonekana kuwa na uwezo hata wa kumaliza Ligi kwenye nafasi ya 3 au 2.

 

Sasa ukishawaza hayo maamuzi magumu ambayo yanaifanya timu iwe salama katika msimamo mpaka sasa, nakuletea hapa juu ya umahiri wa Viongozi wa Singida Big Stars juu ya kuijengea taswira nembo ya Singida Big Stars. Umeshawahi kujiuliza kuna wadhamini wangapi walioko nyuma ya klabu hii? Unadhani ni rahisi kwa klabu iliyopanda tu ligi kuu nembo yake ikafanya vizuri sokoni? Yaani kuwashawishi Airtel na wengineo sio jambo rahisi.

Hapa unatakiwa kuusifu uwezo wa viongozi wa klabu ambao walifanya kazi ya kuwashawishi watu ili wakae karibu na nembo yao. Pia lazima uwasifu viongozi namna ambavyo walipambana kuwafanya wachezaji wenye majina makubwa kujiunga na kuja kuitumikia nembo ile ya klabu, walifanya kazi kubwa sana.

 

Miaka miwili nyuma hapa nchini palikuwa na klabu tatu tu ambavyo kila mchezaji hapa nchini alitamani kucheza, leo hii Singida Big Stars wameongezeka, haya ni mafanikio makubwa. Kwa miezi michache tu tayari wameweza kuwashiwishi watu wawazungumzie.

 

Singida Big Stars naiona wapi? Naiona ikidumu katika soka la ushindani hapa nchini kwa miaka inayokuja. Hii inachagizwa na uthubutu wao wa kufanya sajili nzuri, ambazo zimekuwa gumzo sana. Mwangalie Bruno Gomes unaweza kujiuliza walimtoa wapi huyu? Hapa huwezi kusita kusema nyuma ya taratibu zao za usajili kuna watu makini sana.

 

Asanteni Singida Big Stars mmekuwa kioo kwa vilabu vingine vidogo. Hamjataka kuwa wanyonge ndani ya ligi kama yalivyo mawazo ya timu zingine ndogo. Mmekuwa watu mnaoipambania nembo yenu ifanye vizuri sokoni kiasi cha kuwavutia watu.

 

Hongereni pia kwa Jezi nzuri, jezi ambayo watu wengi wanavutiwa nayo. Uzuri pekee hautoshi bali mipango yenu ya promosheni imewalipa. Hakika vilabu vingine vidogo vina mengi ya kujifunza kwenu.

Singida Big Stars