Baada ya Yanga SC kucheza na Geita Gold FC robo fainali na kufanikiwa kuvuka kwenda hatua ya Nusu Fainali, ni rasmi sasa tutacheza dhidi ya Yanga SC mchezo wa Nusu Fainali hiyo ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Msemaji na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa timu yetu, Hussein Massanza, amesema timu ipo tayari kukabiliana na Yanga licha ya ugumu tutakaokutana nao ikizingatiwa kuwa Yanga ndiye Bingwa Mtetezi wa Kombe hili msimu uliopita.
Massanza amewaambia wanahabari kuwa timu yetu ambayo ilishatangulia hatua ya nusu fainali baada ya kuwafunga Mbeya City kwenye mchezo wa Robo Fainali, ilikuwa ikisubiri kumfahamu mpinzani tutakayekutana nae Nusu Fainali kati ya Yanga na Geita, hivyo sio jambo la kushtukiza kuona Yanga amevuka na ndiye atakuwa mpinzani wetu katika hatua hiyo ngumu.
Mchezo wa Nusu Fainali umepangwa kufanyika katika Uwanja wetu wa nyumbani wa CCM Liti na kinachosubiriwa kwa sasa ni tarehe rasmi ya mchezo huo.
Mwisho Massanza anawataka mashabiki wetu mjiandae kuja kwa wingi kuwasapoti Big Stars katika mchezo huo mgumu na ameweka wazi kuwa malengo ya timu ni kutwaa taji la kombe la Shirikisho la Azam Sports msimu huu.