Main Sponsor

SINGIDA NI TIMU ILIYONIVUTIA ZAIDI – THOMAS ULIMWENGU

Nyota wa zamani wa klabu ya TP Mazembe ya nchini Kongo ambaye kwa sasa amerudi Tanzania kuichezea klabu ya Singida Big Stars, Thomas Ulimwengu, amesema alivutiwa zaidi kujiunga na timu yetu kwa sababu aliona ni timu mpya lakini yenye mwenendo mzuri. Ikumbukwe kuwa Thomas Ulimwengu hakuwahi kuchezea timu yoyote ya Ligi Kuu licha ya mafanikio makubwa aliyoyapata kwenye soka la kulipwa nje ya nchi, hivyo Singida Fountain Gate inakuwa timu yake ya kwanza kucheza kwa timu za nyumbani Tanzania. Aidha, Ulimwengu ametoa maoni yake kuhusu wachezaji wengi wa kigeni wanaosajiliwa kucheza Ligi Kuu ya Tanzania ambapo amesema kwa mtazamo wake anaona wachezaji wengi wao wanafuata malipo mazuri na umaarufu. Akizungumza kupitia mahojiano maalum na chaneli yetu ya YouTube ya BIG STARS TV, Ulimwengu ambaye ni mchezaji mzawa ametolea mfano kwa nchi ya Kongo ambako amecheza na kuishi kwa miaka mingi, amedai huko hakuna matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya michezo ukilinganisha na Tanzania ambavyo kwa kiasi kikubwa vinachangia kukuza majina ya wachezaji. “Mimi naona wachezaji wengi wamefanya (Tanzania) kama ni njia. Wanaona kabisa nikija Tanzania nikifunga magoli kadhaa naondoka.” amenukuliwa Ulimwengu. Sababu nyingine ametaja ni maslahi makubwa ambayo vilabu vya Tanzania vinatoa kwa wachezaji wa kigeni na hivyo kupelekea wachezaji wengi kuvutiwa kuja kucheza nchini. “Klabu za Tanzania zinathamini sana wachezaji wa nje kuliko wazawa. Wanakuja hapa, wanathaminiwa sana wanalipwa vizuri. So hakuna mchezaji ambaye hapendi kwenda kwenye mpira akalipwa vizuri, wanakuja kwa sababu wanaona kuna mafanikio” amefunguka Ulimwengu ambaye ni rafiki wa karibu na Nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mbwana Samatta. Thomas Ulimwengu ametoa wito kwa timu za Tanzania kuthamini wachezaji wazawa kwa sababu wapo wachezaji wenye uwezo mzuri na vipaji vikubwa kuliko baadhi ya wachezaji wa kigeni wanaosajiliwa nchini.

Singida Big Stars